Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuia ya Qawluna wal-Amal, iliandaa hafla ya mshikamano kwa ajili ya kuwaunga mkono wanawake na wasichana wanaovaa hijabu katika Jamhuri ya Azerbaijan, kwa kuungwa mkono na kuhudhuriwa na Sheikh Ahmad al-Qattan, mwenyekiti wa jumuia hiyo.
Mkusanyiko huo ulifanyika katika eneo la Bralias, ukiwahusisha wawakilishi wa idara ya wanawake ya Hizbullah na mashirika ya wanawake ya eneo la Biqaa. Hafla hiyo ilikuwa jibu la wazi na thabiti dhidi ya sera zenye vikwazo katika taasisi za elimu nchini Azerbaijan, ambazo zinawanyima wasichana fursa ya kuendelea na masomo kwa sababu ya kushikamana kwao na hijabu.
Washiriki wa mkusanyiko huo walisisitiza umuhimu wa kulinda heshima na hadhi ya mwanamke, pamoja na haki yake ya msingi ya kupata elimu huku akihifadhi utambulisho wake wa kidini.
Msimamo wa Sheikh al-Qattan: Kuwasaidia Wanaodhulumiwa, Bila Kujali Mipaka
Sheikh Ahmad al-Qattan, mwenyekiti wa jumuia hiyo, alisisitiza katika hotuba yake kwamba hatua hii inatokana na mafundisho ya Qur’ani Tukufu na ni wajibu wa kimaadili wa kumsaidia kila mtu anayekabiliwa na dhuluma, popote pale duniani.
Aliongeza kuwa suala la Azerbaijan si jambo la ndani ya nchi hiyo pekee, bali ni mtihani wa mshikamano wa Umma wa Kiislamu. Alisema: “Tunaitazama migogoro inayowakabili wanaodhulumiwa kwa mtazamo mpana na kwa hisia ya kuwajibika, hivi ndivyo tulivyosimama dhidi ya uhalifu unaofanyika nchini Lebanon, Ghaza na Yemen.”
Aidha, akizungumzia shinikizo linazowakabili wananchi wa kusini mwa Lebanon na Palestina, alibainisha kuwa; utetezi wa haki na uadilifu haupaswi kuathiriwa na mahesabu ya kisiasa au shinikizo kutoka nje. Alisisitiza kwamba amani na utulivu vinaweza kupatikana tu kupitia kulinda haki na heshima ya binadamu.
Manal al-Qattan: Hijabu ni Utambulisho, Siyo Chombo cha Ubaguzi
Manal al-Qattan, mwenyekiti wa shirika la wanawake, katika hotuba yake iliyozingatia mitazamo ya kisheria na kijamii, aliitambulisha hijabu kuwa ni zaidi ya vazi, bali ni “imani na utambulisho.” Akizungumzia picha za kuhuzunisha za wasichana na walimu wanaokaa wakilia mbele ya milango iliyofungwa ya shule alisema kuwa; marufuku ya hijabu kwa hakika ni kuwanyima wanawake haki yao ya kupata elimu na kujaribu kuwaondoa katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Akikosoa msimamo wa serikali ya Azerbaijan, alisisitiza kwamba; mfumo wa utawala wa kisekula haupaswi kugeuzwa kuwa chombo cha kuwaondoa watu wenye misimamo ya kidini au kuleta ubaguzi katika elimu.
Al-Qattan alizitaka taasisi za kimataifa, zikiwemo Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu na Umoja wa Mataifa, kuingilia kati haraka ili kulinda haki za msingi za wanawake Waislamu dhidi ya sera hizi zinazokiuka misingi inayopaswa kuongoza jamii.
Mkusanyiko huo ulimalizika huku washiriki wakisisitiza kuendelea na juhudi za kupigania kurejeshwa wanafunzi wanaovaa hijabu madarasani.
Hatua hii ilionyesha kwamba; sauti ya wanawake Waislamu dhidi ya sera zenye vikwazo ni sauti ambayo, kwa kutegemea utambulisho wa kidini na haki za binadamu, inazidi kugeuka kuwa harakati ya kuelimisha na kuhamasisha uelewa katika ngazi ya kikanda.
Maoni yako